Mzozo wa Tanzania na Malawi kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa umezidi kuchukua sura mpya baada ya Serikali ya Tanzania kupinga kauli ya Rais wa Malawi, Joyce Banda aliyetangaza kujitoa nchi yake katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo baada ya kubaini kuwa Dar es Salaam imezindua ramani mpya inayogusa mipaka ya ziwa hilo. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema, mabadiliko ya ramani ya taifa hayahusiani na mgogoro wa Malawi na Tanzania katika Ziwa Nyasa. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Tanzania imebainisha kwamba, ni kweli kuna mabadiliko ya ramani ya taifa lakini mabadiliko haya yanatokana na kuongezeka kwa mikoa na wilaya mpya na kwamba, mipaka ya nchi katika mabadiliko ya ramani hii imebaki kama ilivyokuwa enzi za ukoloni. Hivi karibuni Malawi ilitangaza kujitoa katika mazungumzo na jirani yake huyo, uamuzi ambao umekwenda sambamba na kufutwa kwa safari ya Rais Banda nchini Tanzania, hatua ambayo inazidisha mgogoro baina ya nchi hizo mbili. Tayari Rais Joyce Banda wa Malawi ametangaza kuwa, nchi yake itawasilisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) mzozo wake wa mpaka na Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment