Baadhi
ya abiria wakiingia kwenye treni wakati wa uzinduzi rasmi wa usafiri wa
treni kutoka Ubungo mpaka Stesheni jijini Dar es salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (katikati) akiwasili kupanda treni kituo cha tazara kuelekea mjini kufanya uzinduzi
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndani ya treni
…………………………………………….
USAFIRI wa kutumia treni jijini
Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la
Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza leo. Treni ya kwanza
imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati ya jiji,
ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetumia
wastani wa dakika 30 kufika katikati ya jiji.
Treni ilioanza kazi leo iliyokuwa
na injini mbili (vichwa vya traini) moja ikiwa imefungwa nyuma na
nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria wa
kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba
wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu huku wanafunzi wakitakiwa
kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo ambao ni wamajaribio, akiwa
pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli.
Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya TAZARA ambayo itafanya
kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea
Mwakanga.
Akizungumza mara baada ya
ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni hiyo inaendelea
kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es Salaam ambao
wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni, ambapo utumia
muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini.
Alisema jumla ya mabehewa ya
treni 14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na mafundi wazalendo
nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya kusafirisha abiria
kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa
inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa
zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi
na nyingine ikienda.
Akifafanua zaidi alisema kitendo
cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa
kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia sh.
bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali ingelazimika kukodi injini gharama
ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh.
milioni moja kwa siku.
Hata hivyoDk. Mwakyembe amewataka
Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa upungufu utakaojitokeza kwa
safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya marekebisho kadhaa,
lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. Mwandishi wa habari hizi
alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo.
Awali akizungumza mmoja wa
viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo itafanya kazi kila siku
isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na itaanzia saa 12:00 asubuhi
hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa 9:00 za jioni,
itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne usiku.
Uchunguzi uliofanywa na muandishi
wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la treni linauwezo wa kuchukua
abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango minne, feni, taa, muziki/redio,
pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa abiria ambao watakuwa
wamesimama.
Aidha mabehewa yote yana
madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha. Treni ilioanza
kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la Mwananchi
(relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo Gerezani
(Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha
Polisi Kati (Katikati ya Jiji).
*Imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
*Imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment