Jeshi la Polisi la Tanzania limekataa kutoa dhamana kwa Sheikh Ponda
Issa Ponda Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Tanzania
ambaye jana alitiwa mbaroni na jeshi la polisi nchini humo kwa tuhuma
kadhaa za kutenda jinai. Taarifa za awali zilieleza kuwa, Sheikh Ponda
anatuhumiwa kuwa amehamasisha maandamano kwenda Wizara ya Mambo ya
Ndani, uvamizi wa kiwanja cha Chang'ombe, maandamano kidongo chekundu na
hali kadhalika vurugu zilizotokea hivi karibuni Mbagala. Duru za karibu
na jumuiya za Kiislamu Tanzania zimeeleza kuwa, jeshi la polisi
lilimuhoji Sheikh Ponda kwa masaa kadhaa, na hatimaye kukataa kumpa
dhamana mtuhumiwa huyo. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam
Afande Suleiman Kova amesema kuwa, mtuhumiwa huyo hawezi kupewa dhamana
hadi pale yatakapofanyika mashauriano ya kina na ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka DPP. Afande Kova amesema kuwa, uchunguzi wa vurugu za Mbagala
bado unaendelea, kwani kuna uwezekano wa kuunganishwa Sheikh Ponda na
watuhumiwa wengine waliofanya uhalifu na uporaji Mbagala. Hata hivyo
ripoti tulizopokea hivi karibuni zinaeleza kuwa, Sheikh Ponda na wenzake
waliokamatwa leo wamesomewa shitaka moja tu ambalo ni la kuvamia
kiwanja kilichopo Chang'ombe. Baada ya kukataliwa dhamana, washtakiwa
hao wamerejeshwa rumande na kesi yao imepangwa kusikilizwa tarehe Mosi
Novemba mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment