Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amesema kuwa lengo lake kuu ni
kuendesha uchaguzi kote nchini humo ifikapo mwezi Machi mwakani kwa
mujibu wa katiba mpya ya nchi hiyo. Mugabe amesema kuwa harakati zao
zinapasa kusonga mbele licha ya mitazamo yao ya kisiasa kutofautiana.
Mugabe ameyatamka hayo katika kikao kilichohudhuriwa pia na Morgan
Tsvangirai Waziri Mkuu wa Zimbabwe na ambaye pia ni mpinzani wake mkuu
wa kisiasa. Kamati ya katiba ya Zimbabwe imesaini rasimu ya mwisho ya
katiba hiyo mpya na kuidhinishwa na karibu mirengo yote mikuu ya kisiasa
na kiraia ya nchi hiyo, hata hivyo tarehe ya kufanyika kura ya maoni
kuhusiana na katiba hiyo bado haijatangazwa. Kura ya maoni ndiyo
itakayofungua njia ya kufanyika chaguzi zijazo za Rais na Bunge huko
Zimbabwe.
Mfumuko wa bei Kenya umepungua kwa kiasi cha chini zaidi katika
kipindi cha miezi 23 iliyopita na hivyo kuibua matumaini miongoni mwa
wananchi.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Kenya (KNBS), pamoja na
kuwepo ongezeko la bei ya mafuta ya petroli, mfumuko wa umeshuka hadi
asilimia 4.14 mwezi Oktoba ikilinganishwa na asilimia 5.32 mwezi
Septemba mwaka huu. Kiwango cha mfumuko wa bei Kenya sasa ni cha chini
zaidi tokea Desemba mwaka 2010.
Katika taarifa kaimu mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Kenya
Zachary Mwangi amesema kumeshuhudiwa kushuka bei ya vyakula kama vile
sukuma wiki,mahindi, tomato na karoti. Hatahivyo amesema kumeshuhudiwa
ongezeko la bei ya baadhi ya bidhaa kama vile viazi, ndizi na nyama ya
ng’ombe.
Weledi wa mambo wanasema mfumuko wa bei umepungua Kenya kutokana na
ongezeko la uzalishaji wa vyakula, kupungua bei ya petrol kimataifa
katika mizi iliyotnagulia na usimamizi bora ya kifedha.