Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina
Faso amesema nchi yake iko tayari kushiriki katika oparesheni ya kijeshi
huko kaskazini mwa Mali.
Jibril Bassole amesisitiza juu ya
kukombolewa eneo la kaskazini mwa Mali na kusema kuwa wanajeshi wa
Burkina Faso wako tayari kushiriki kwenye oparesheni hiyo. Burkina Faso,
Niger na Mauritania ni nchi jirani na Mali ambazo zimeathirika zaidi na
na mgogoro wa kisiasa, kibinadamu na kiusalama huko kaskazini mwa nchi
hiyo. Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imetoa mamilioni ya
dola kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi tangu mwanzoni mwa mwaka huu
baada ya raia wa kaskazini mwa Mali kulikimbia eneo hilo na kuelekea
katika nchi jirani. Uhaba wa chakula na ukosefu wa amani katika eneo la
Sahel-Sahara la Afrika umekuwa changamoto kuu kwa nchi za eneo hilo.
Katika mazingira hayo, Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya ya kieneo ya
Ecowas zimeafiki suala la kuanzishwa operesheni ya kijeshi ili
kulikomboa eneo la kaskazini mwa Mali linalodhibitiwa na makundi yenye
silaha. Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katikati ya mwezi
huu liliwasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ripoti
inayoidhinisha oparesheni hiyo.
Katika hali ambayo wakuu wa AU, ECOWAS
na jamii ya kimataifa wanasubiri azimio la Baraza la Usalama kuhusiana
na kadhia ya kaskazini mwa Mali, Ban Ki Moon Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa pia ameafiki kwa masharti kutumwa wanajeshi nchini humo. Mpango
wa kutuma vikosi vya jeshi chini ya uongozi wa nchi za Kiafrika ili
kuiunga mkono serikali ya Mali utajulikana kwa kifupi kwa jina la
Afisma. Ban Ki Moon ameeleza kuwa mazungumzo ya pande zote na makundi
yanayobeba silaha yenye mfungamanao na makabila ya Tuareg huko kaskazini
mwa Mali yanapasa kufanyika kwanza na oparesheni ya kijeshi iwe chaguo
la mwisho la kutatua mgogoro wa Mali.
Wakati huo huo ripoti mbalimbali
zinaeleza kuwa makundi yenye silaha ya kusini mwa Mali yanawachochea
vijana kutoka nchi za Ulaya na za Kiafrika. Makundi hayo ambayo mwaka
1999 yalipambana na jeshi la Mali hivi sasa yanajipanga upya ili
kuyakomboa maeneo ya kaskazini chini ya nara" Mali ni Nchi yetu". Licha
ya kuweko uhaba mkubwa wa idadi ya wanajeshi katika jeshi la Mali,
lakini makundi yenye silaha huko kusini mwa nchi hiyo yanajizuia
kujiunga na jeshi na yameazimia kukomboa eneo la kaskazini kwa mapambano
yao wenyewe.
Huko kaskazini mwa Mali harakati ya
Kitaifa ya Ukombozi wa Azawad ambayo kwa miaka kadhaa inaendesha
mapigano dhidi ya jeshi la Mali kwa ajili ya kulikomboa eneo la Azawad
hivi sasa imetengwa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa wapiganaji wa baadhi
ya makundi ya kaskazini mwa Mali kama harakati ya Jihad na Uadilifu ni
raia kutoka katika nchi za Algeria, Tunisia, Misri, Sudan na Pakistan
pia.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa
biashara haramu ya madawa ya kulevya, silaha na binadamu katika eneo la
Sahel-Sahara imeongezeka tangu kuanza mgogoro wa Mali. Mgogoro wa
kaskazini mwa Mali na machafuko ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo ni miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa katika
mazungumzo ya hivi karibuni huko Washington kati ya Bi Nkosazana Dlamini
Zuma, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Hillary Clinton Waziri wa
Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Naibu wake John Carson.
No comments:
Post a Comment