Watu 24 wameuawa katika mapigano
kati ya jeshi la Sudan Kusini na wapiganaji wa kundi la wanamgambo
linaloongozwa na mtu aliyejitangazia unabii katika jimbo la Jonglei huko
mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa
liliwashambulia waasi hao wanaoongozwa na Dak Kueth ikiwa ni sehemu ya
kampeni ya kuwatomokeza wanamgambo wa makundi ya kikabila katika eneo
hilo. Luteni Jenerali Kuol Deim Kuol amesema wanamgambo 19 na askari
watano waliuawa katika mapigano hayo.
Mfululizo wa mauaji ya ulipizaji
kisasi kati ya makabila ya Murle na Lou Nuer yanayochochewa na wizi wa
mifugo yamekuwa yakishuhudiwa huko Jonglei huku serikali ya Juba
ikiendesha kampeni ya upokonyaji silaha katika maeneo mbali mbali ya
nchi hiyo. Kwa mujibu wa Kuol walipata taarifa kuwa Dak Kueth alikuwa
anawahamasisha vijana wa Lou Nuer kwenda kuwashambulia watu wa kabila la
Murle huko Akobo ndipo wakaamua kufanya shambulio la kuzuia kutokea
hujuma hiyo. Hii ni katika hali ambayo makundi ya kutetea haki za
binadamu yanalilaumu jeshi la Sudan Kusini kuwa lilifanya jinai mbali
mbali ikiwemo ubakaji na utesaji wakati wa kutekeleza kampeni yake ya
upokonyaji silaha mapema mwaka huu…/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment