Wakili anayewatetea viongozi wa
muungano wa taasisi za Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho visiwani
Zanzibar amesema kuwa, viongozi hao wameanza kupatiwa huduma muhimu kama
mahabusu wengine katika gereza la Kiinua Mguu mjini Unguja.
Bw. Salum Taufiq amenukuliwa akisema
hayo na kuongeza kuwa, wateja wake tayari wameruhusiwa kula chakula
kutoka nyumbani, kusoma Qur'ani misahafuni, kubadilisha nguo pamoja na
kutoka kwenye vyumba vyao na kuchanganyika na mahabusu wengine.
Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili
viongozi hao ni kusababisha uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa
taifa na wako kizuizini kwa miezi kadhaa sasa.
Viongozi hao ni maarufu kwa kupigania
mabadiliko katika muundo wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar na
walifanya mikutano mingi kuhamasisha wananchi kukataa mfumo wa hivi sasa
wa muungano wa nchi hizo mbili wakisema kuwa si wa kiadilifu.
Viongozi hao wa Uamsho pia wamefungua
kesi ya kupinga kubaguliwa na kutopewa huduma bora tangu walipofunguliwa
mashtaka tarehe 21 Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo upande wa mashtaka umepinga
madai hayo na kuitaka Mahakama Kuu ya Zanzibar, kutupilia mbali kesi
hiyo iliyofunguliwa na viongozi wanane wa Uamsho, ukidai kwamba kesi
hiyo imefunguliwa kinyume cha sheria kutokana na hati ya kiapo kukosa
tarehe ya kufunguliwa pamoja na jina la mtu aliyekula kiapo kwa niaba ya
washitakiwa hao.
Sheikhe Farid Hadi Ahmed, Sheikh Mselem
Ali Mselem, Sheikh Mussa Juma Issa, Sheikh Azzan Khalid Hamdan, Sheikh
Suleiman Juma Suleiman, Sheikh Khamis Ali Suleiman, Sheikh Hassan Bakari
Suleiman na Sheikh Gharib Ahmada Omar ndio waliofungua kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment