Social Icons

rss feed facebook twitter google plus linkedin youtube email

Wednesday, December 26, 2012

Padri Ambros Mkenda apigwa risasi Zanzibar



Padri Ambros Mkenda apigwa risasi ZanzibarWatu wasiojulikana wamempiga risasi Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar na kumjeruhi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Juma Muhammed amethibitisha tukio hilo huku jeshi la polisi likiendelea kuchunguza ili kubaini wahusika wa uhalifu huo.  Askofu Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini alidai hivi karibuni kumekuwepo vipeperushi vilivyosambazwa vikiwatisha watu wenye imani ya Kikristo na kuiomba serikali iongeze ulinzi na kuimarisha usalama. Aidha ameiomba serikali kuchukua hatua za tahadhari kwani matukio kama hayo yameanza kutokea kwa viongozi wa dini kuanzia kwa Sheikh Soraga aliyemwagiwa tindikali na hivi sasa Padri Ambros.
Hata hivyo Kamanda Aziz Muhammed amekanusha madai hayo na kusema kuwa wanalichukulia tukio hilo kuwa la kawaida tu la kihalifu na pia kuongeza hawana vipeperushi vya aina yoyote vinavyoelezea kutishwa viongozi wa kidini wala hawaamini kwamba matukio hayo yanafanywa dhidi ya dini fulani. Ameongeza kuwa, Padri Ambros ni mhasibu kanisani na kwamba huenda hiyo ndiyo sababu iliyopelekea kushambuliwa na wahalifu waliodhani kuwa amebeba pesa.

No comments:

Post a Comment