Serikali ya Mali na makundi mawili
ya waasi yaliyodhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo mwezi Aprili
mwaka huu yamekutana kwa mara ya kwanza na kukubaliana kufanya
mazungumzo ili kuhitimisha mgogoro nchini humo. Hayo yameelezwa na
waziri kutoka nchi mpatanishi Burkina-Faso.
Ujumbe wa serikali ya Mali
jana ulikutana na wawakilishi wa kundi la kabila la Tuareg linalopigania
kujitenga huko kaskazini mwa Mali ambalo uasi wake wa awali ulitekwa
nyara na kundi la Ansaruddin lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida.
Kundi hilo la Ansaruddin liliwakilishwa pia na wajumbe wake katika
mkutano wa Ouagadougou mji mkuu wa Burkina-Faso.
Djibril Bassole Waziri wa Mambo ya Nje
wa Burkina-Faso amesema kuwa jumbe hizo tatu zimekubaliana kwamba kuna
haja ya kuanzishwa fremu ya mazungumzo ya kitaifa ya Mali kwa
kuwashirikisha wawakilishi wa jamii mbalimbali zinazoishi huko kaskazini
mwa Mali. Pande hizo tatu zimesema baada ya kumaliza mkutano wao kuwa
zimekubaliana kumaliza uhasama kati yao.
No comments:
Post a Comment